Ijumaa 6 Februari 2026 - 07:00
Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini India, latangaza tamko la kumuunga mkono Ayatullah Khamenei

Hawz/ Baraza la Wanazuoni wa Kishia India, limetoa tamko rasmi kulaani vikali vitisho vya hivi karibuni vya Donald Trump dhidi ya Ayatullah Sayyid Ali Husayni Khamenei (Mola amlinde), kiongozi mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kumtaja kuwa “mapigo ya moyo kwa waliodhulumiwa duniani na tumaini la Wapalestina wanaodhulumiwa.”

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Baraza la Wanazuoni wa Kishia India katika tamko lake rasmi lililotoa, lililaani kwa maneno makali vitisho vya Donald Trump dhidi ya Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei (Mwenyezi Mungu adumishe baraka zake), kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kumtaja kuwa “ni mapigo ya moyo kwa waliodhulumiwa duniani na tumaini la Wapalestina wanaodhulumiwa.”

Matini ya tamko hilo ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote, na rehema na amani zimshukie bwana wetu Muhammad na Ahlul-Bayt wake watoharifu.

Leo dunia, hususan umma wa Kiislamu, uko katika moja ya vipindi nyeti na vya kuamua hatima yake katika historia. Nguvu za kibeberu, kwa kupuuza misingi ya kielimu, kibinadamu na sheria za kimataifa, na kwa kutegemea nguvu na kiburi — hasa Marekani pamoja na mshirika wake wa Kizayuni Israel — zimeweka usalama na amani ya dunia katika hatari.

Vitisho na njama dhidi ya marji' mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu, faqihi mtukufu na kiongozi wa Waislamu, kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, havimlengi mtu mmoja tu, bali ni shambulio la wazi dhidi ya heshima na utambulisho wa umma wa Kiislamu. Hatua hii si tofauti ya kisiasa tu, bali ni tangazo la uadui wa wazi dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu si kiongozi wa kisiasa wa nchi moja tu, bali pia ni marji' wa kidini na faqihi anayetambuliwa na Waislamu na watu huru duniani kote. Sauti ya kuikomboa Quds Tukufu, matumaini ya Wapalestina wanaodhulumiwa, na faraja ya mataifa ya muqawama ya Lebanon, Yemen na Iraq, vimefungamana na uongozi wake wa hekima. Mwenendo na busara yake hutufundisha kwamba mbele ya dhulma, njia ya watu wa imani si kusalimu amri, bali ni kusimama kwa uelewa, subira, hekima na umoja.

Tamko hilo linaendelea kusema kwamba; Baraza la Wanazuoni wa Kishia India, kwa kuhisi wajibu wake kikamilifu, linatangaza kuwa tishio lolote dhidi ya kiongozi huyo mkuu kwa hakika ni changamoto dhidi ya umma wote wa Kiislamu, na mtazamo huo uko kinyume wazi na maadili ya kibinadamu, misingi ya kimataifa na mafundisho ya Kiislamu.

Tamko hilo linahitimishwa kwa wito wa pamoja: wanazuoni, wasomi, shakhsia za kisiasa na kijamii, pamoja na watu wote huru na wenye dhamiri hai, wanahimizwa — bila kujali tofauti za kimadhehebu na kimtazamo — kulaani dhulma hii kwa sauti moja na kusimama imara katika haki na uadilifu. Mwishoni, iliombwa dua kumuombea afya, heshima na mafanikio zaidi kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu aupe umma wa Kiislamu umoja na kuwapa waliodhulumiwa nusura na ushindi wa haraka.

Hujjatul-Islam Jawad Haidar Rizvi,
Baraza la Wanazuoni wa Kishia India.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha